Saratani ya mlango wa uzazi ni mojawapo ya saratani zinazoweza kuzuilika zaidi. Uchunguzi wa mara kwa mara wa mlango wa uzazi ni njia bora zaidi ya kujikinga kutokana na saratani ya mlango wa uzazi.
Kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi ni nini?
Kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi huangalia afya ya mlango wa uzazi wako. Daktari au muuguzi atachukua sampuli ndogo kutoka kwa mlango wa uzazi kwa kutumia usufi - kama pap smear - na kuipima kwa virusi ya papilloma ya binadamu (HPV)
HPV ni virusi vya kawaida ambavyo vinaweza kubadilisha seli kwenye mlango wa uzazi wako. Ni chanzo cha kawaida zaidi cha saratani ya mlango wa uzazi.
Watu wengi wenye HPV hawana dalili, ndio maana uchunguzi ni muhimu.
Ikiwa kipimo chako kinaonyesha kuwa una HPV, huchukua miaka 10 au zaidi kwa HPV kukua saratani ya mlango wa uzazi. Ni nadra kwa maambukizi ya HPV kugeuka kuwa saratani ya mlango wa uzazi.
Mchoro wa mfumo wa uzazi wa mwanamke
Je, unahitaji kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi?
Unahitaji kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi ikiwa wewe:
- ni mwanamke au mtu aliye na mlango wa uzazi
- una umri wa miaka 25 hadi 74
- umewahi kushiriki ngono na mtu mwingine, licha ya jinsia au utambulisho wa kijinsia.
Ni muhimu kupimwa, hata kama umepata chanjo ya HPV. Ingawa chanjo ya HPV ni nzuri sana, haizuii maambukizi yote ya HPV.
Je, unahitaji kupata vipimo vya uchunguzi wa mlango wa uzazi mara ngapi?
Unahitaji kupimwa kila baada ya miaka mitano kati ya umri wa miaka 25 na 74.
Kufanya uchunguzi kila baada ya miaka mitano ni salama. Hii ni kwa sababu njia ya zamani ya kupima kila baada ya miaka miwili (pap smear) ilipima tu mabadiliko katika seli za mlango wa uzazi. Vipimo vipya vya uchunguzi wa mlango wa uzazi vya HPV, ambavyo vinaweza kusababisha mabadiliko katika seli za mlango wa uzazi. Hii husaidia kugundua mabadiliko mapema.
Je, unaweza kupata kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi wapi?
Vipimo vya uchunguzi wa mlango wa uzazi vinapatikana katika kliniki za daktari, vituo vya afya na kliniki za kupanga uzazi.
Je, kipimo cha uchunguzi wa mlango wa uzazi kinafanya wapi?
Ikiwa mtoaji wa huduma ya afya anachukua sampuli
Ikiwa mhudumu wako wa afya akichukua kipimo, utahitaji kuvua nguo chini ya kiuno na ulale chali huku magoti yako yakiwa yamepanuka. Utapewa shuka ili ujifunike.
Ataingiza polepole kifaa cha uchunguzi kiitwacho spekulum (kifaa chenye umbo la bili ya bata) kwenye uke wako na kutumia brashi ndogo kuchukua sampuli ya seli kutoka kwenye mlango wa uzazi wako. Hii inaweza kukufanya usihisi sawa, lakini haifai kuumiza. Unaweza kuomba mhudumu wa afya wa kike ukipenda..
Ikiwa unachukua sampuli yako mwenyewe (kujichukulia sampuli)
Ukiamua kuchukua sampuli yako mwenyewe, utahitaji kufanya hivyo katika kituo chako cha afya. Mhudumu wako wa afya ataeleza jinsi ya kuchukua kipimo hicho. Unaweza kufanya hivyo faraghani au umwombe akusaidie.
Kujichukulia sampuli kunahusisha kuingiza kifaa cha uchunguzi (swab) kwenye uke wako. Sogeza polepole kifaa cha uchunguzi katika mwendo wa mviringo kwa sekunde 10 hadi 30. Hii inaweza kukufanya usijisikie vizuri, lakini haifai kuumiza. Ndipo ondoa kifaa cha uchunguzi kutoka kwenye uke wako na kukirudisha kwenye kifungashio ulichopewa.
Kujichukua sampuli mwenyewe ni salama na sahihi kama vile tu mhudumu wa afya akichukua sampuli yako.
Ni nini hufanyika baada ya kupimwa?
Baada ya sampuli yako kuchukuliwa, hutumwa kwa maabara ili kupimwa.
Kama kipimo chako haonyeshi HPV, unaweza kungoja miaka mitano kwa kipimo chako kijacho.
Kama kipimo chako kikionyesha HPV, mhudumu wako wa afya atazungumzia nawe kuhusu unahitaji kufanya nini. Matokeo yako yatatumwa katika Rejesta ya Kitaifa ya Uchunguzi wa Saratani (NCSR). Huduma hii pia itatuma ujumbe wa kukumbusha kwako kuhusu siku ya kupimwa tena.
Wakati wa kumwona daktari wako
Mwona daktari wako au mtoaji huduma wa afya yako ikiwa huna hakika kwamba kipimo kijacho chako cha uchunguzi wa mlango wa uzazi kitakuwa siku gani.
Ikiwa unapata kutokwa na damu, maumivu au utoko isiyo ya kawaida ukeni, umwone daktari wako mara moja. Kumbuka, kujichukua sampuli hapendekezwi ikiwa una dalili zozote hizi.
Mwulize daktari wako kuhusu chanjo ya HPV ikiwa bado hujaipata.
Kupata maelezo, nyenzo na rufaa zaidi, tembelea jeanhailes.org.au/health-a-z/health-checks/cervical-screening-test.
© 2024 Jean Hailes Foundation. All rights reserved. This publication may not be reproduced in whole or in part by any means without written permission of the copyright owner. Contact: licensing@jeanhailes.org.au